Tanzania itashiriki kambi ya Basketball Without Borders (BWB) na mchezo wa NBA itakayofanyika Pretoria, Afrika Kusini tarehe 1-4 August, 2018.

Msafara wa Tanzania utaongozwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) Ndg. Phares Magesa, ambaye ataambatana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar Es Salaam (BD) Ndg. Okare Emesu, Kocha Timu ya Taifa ya Vijana Ndg. Bahati Mgunda, mchezaji wa kiume Ndg. Atiki Ally Atiki na  mchezaji wa kike Ndg.Jesca Ngisaise Onga’anyi.

Mchezo wa NBA Africa 2018, utakuwa ni kati ya Team Africa vs. Team World, na utafanyika August 4 saa 11 jioni, Sun Arena, Time Square.

Huu utakuwa ni mchezo wa tatu wa NBA kufanyika Afrika baada ya wa kwanza uliofanyika mwaka 2015, Ellis Park Arena (Johannesburg) na wa pili uliofanyika 2017, TicketPro Dome (Johannesburg).

Mchezo huu unafanyika kuunga mkono jitihada za The Nelson Mandela Foundation na kusherehekea miaka 100 ya Nelson Mandela.

Mchezo huo utahudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wachezaji wa NBA (NBA) Michele Roberts na Kamishna Mkuu wa NBA Adam Silver, Balozi wa heshima wa NBA  Dikembe Mutombo (Democratic Republic of the Congo), Wachezaji wa zamani wa NBA Wayne Embry na wa WNBA Swin Cash, Astou N’Diaye na Ruth Riley.

Michezo hii itaonyesha duniani kote mubashara na TV ya Kwesé, na kurushwa pia na SABC na ESPN2.

Pia kutakuwa na burudani nyingi zitakazoletwa na timu za NBA na vikundi vyao vya burudani kama Bango the Buck (Milwaukee Bucks), Slamson the Lion (Sacramento Kings), the Brooklyn Nets Team Hype Dunkers na  the Utah Jazz Stunters.

Kutakuwa na kambi ya mafunzo ya wachezaji vijana kutoka nchi zote za Afrika itayofanyika kuanzia 1-4 August, 2018 katika shule ya Kimataifa ya Marekani iliyoko Johannesburg. Na kutakuwa na michezo ya wachezaji nyota Vijana wa kike na wa kiume wa Afrika tarehe 4 August, 2018 kabla ya mchezo wa NBA.

Vijana watakaofanya vizuri katika kambi hii watakuwa na nafasi nzuri za kupata nafasi zaidi za majaribio ya kuingia NBA kupitia NBA Academy au NCAA au Ligi kubwa za Ulaya za Kikapu na hatimaye kucheza NBA miaka ya baadae kama wakifanikiwa.

Pia TBF na Chama Cha Mpira wa Kikapu Nchini Marekani (NBA) tutapata nafasi ya kufanya mazungumzo yenye lengo la kuimarisha ushirikiano ili kukuza mchezo wa kikapu nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuongeza wigo wa Junior NBA League ili ichezwe pia mikoa mingine, pia tutazungumzia kupata nafasi zaidi za mafunzo ya vijana wadogo (Basketball Clinics) zinazoendeshwa na NBA sehemu mbalimbali duniani na kuona uwezekano wa kuandaa moja ya matukio makubwa ya NBA ili yafanyike hapa Tanzania, tutawaeleza jitihada zinazoendelea ambapo sasa hamasa ya mchezo imepanda zaidi, Ligi za RBA, Ligi za Kanda na michezo ya kikapu inachezwa karibu kila mkoa Tanzania Bara na Visiwani na pia jitihada za ujenzi wa viwanja kwa Program inayoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Paul Makonda ya kujenga viwanja vipya vitano ambapo kila wilaya itapata kiwanja kimoja cha ndani na pia Waziri wa Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye nae kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano ameahidi kuufanyia matengenezo makubwa uwanja wa ndani wa Taifa uliopo wakati tunasubiri ujenzi wa Uwanja mpya mkubwa wa ndani wa kisasa.

Tutawaeleza wenzetu wa NBA, FIBA na wadau wengine watakohudhuria matukio haya ya Afrika Kusini jitihada hizi na nyingine zinazoendelea ili kubadilisha nao uzoefu kwa lengo la kusaidia kunyanyua mchezo wa kikapu nchini ili mchezo huu nao uwe na mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi yetu.

Tuwaombee vijana wetu hawa waliopata nafasi hii wafanye vizuri kwenye kambi hii ya mafunzo na hatimaye siku za baadae waweze kuwa nyota wetu wa Kimataifa.