Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb) leo tarehe 22 Machi, 2018 amekutana na wadau mchezo wa Mpira wa Kikapu wa Mkoa wa Mbeya. Dkt. Mwakyembe amewapongeza viongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu cha Mkoa kwa kuwezesha timu ya Mkoa wa Mbeya kuwa na rekodi nzuri ya ushindi wa Taifa Cup kwa miaka 3 mfululizo.

Dkt. Mwakyembe aliyeongozana viongozi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mbeya, alizipokea changamoto zilizowasilishwa na Chama zikiwemo uhaba wa walimu wa michezo, uhaba wa vifaa, kukosekana kwa viwanja vya michezo vya ndani na uhaba wa fedha za maandalizi na kuendesha mashindano.

“Hongereni sana timu ya Mpira wa Kikapu ya Mkoa wa Mbeya kwa kuendeleza utamaduni wenu wa kuwa mabingwa wa Taifa Cup kwa miaka 3 mfululizo licha ya kuwa na changamoto lukuki, tumezipokea changamoto zenu na tutafuta njia mwafaka za kuzitatua” alisisitiza Dkt. Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe alitembelea pia kiwanja kinachotumiwa na timu ya mpira wa kikapu ya mkoa kwenye kituo cha Vijana wa Kikatoliki kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya.